KAULI ya Rais John Magufuli kwamba Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein hapaswi kushirikiana na wapinzani, hasa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hammad imepokewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya wasomi na wanasiasa wakieleza kuwa inaweza kuongeza mpasuko wa kisiasa visiwani humo.
Juzi wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa kushukuru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais katika Viwanja wa Demokrasia Unguja, Rais Magufuli alitumia muda mwingi kuzungumzia siasa za Zanzibar na kuwaponda wapinzani, kikiwamo kitendo cha Maalim Seif kumnyima mkono Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
“Juzi wote tulishuhudia msibani na Watanzania wameona kwenye picha, Dk Shein kwa unyenyekevu alimsalimu mtu fulani, lakini akakataa. Mkono huohuo ambao ameukataa, ndiyo Rais Shein anautumia kusaini fedha za safari na matibabu.” alisema Rais Magufuli na kuendelea;
“Kweli una moyo wa upendo, natamani ningekuwa na hata robo maana mimi nisingeweza kutumia mkono wangu kumsainia mtu akatibiwe, wakati mkono huohuo aliukataa.”
Kuhusu wapinzani, Rais Magufuli alisema hawezi kumuingiza mpinzani kwenye Serikali yake kama alivyofanya Dk Shein na kufafanua kuwa ndani ya Serikali yake, hatakuwa tayari kumuingiza mpinzani afanye naye kazi.
Kwa nyakati tofauti jana, wasomi na wanasiasa walisema, kwa hali ilivyo Zanzibar, Rais Magufuli alipaswa kusaidia kuleta mwafaka katika mpasuko wa kisiasa uliopo badala ya kutoa kauli inayoweza kuongeza mpasuko.
CUF yatoa tamko
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama hicho kimesikitishwa na kauli hizo za Rais alizoziita za uchochezi, kupandikiza chuki na uhasama miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
“Kutokana na hadhi ya taasisi yake (Urais), CUF imesikitishwa na Rais kutoa kauli za kuwagawa wananchi na kutaka kujenga chama chake kwa njia ya vitisho na kutumia vyombo vya dola,” alisema Mtatiro.
Kiongozi huyo wa CUF alisema kauli hiyo ya rais Magufuli ni mwendelezo wa kauli kadhaa alizowahi kutoa huku nyuma akihamasisha matumizi makubwa ya kijeshi yasiyozingatia sheria kwa wananchi wa Zanzibar.
“CUF haitakuwa tayari kumwona (Rais) anaiingiza nchi katika mgawanyiko, vitisho na visasi vinavyoweza kuzaa machafuko. Ifahamike kwamba wananchi hawakumchagua kwa ajili ya kuyaandaa majeshi yapambane nao,” alisema.
Wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ali alisema viongozi wote waliopita na Rais Magufuli wanajua chanzo cha mgogoro wa Zanzibar, lakini wanafumbia macho na kuhangaika na mambo yasiyo na msingi.
Dk Bashiru alisema viongozi hao wanajaribu kuaminisha jamii kuwa mgogoro wa Zanzibar ni uchaguzi jambo ambalo si kweli na kuwataka wanasiasa waache malumbano yasiyokuwa na tija katika majukwaa ya kisiasa.
“Unajua tatizo la Zanzibar linahitaji mazungumzo na si jazba wala ukali kwani ni tatizo halisi si la kuktengeneza kama wanavyofanya wanasiasa na kuchukulia ni mtaji wa kisiasa,” alisema.
Alisema mgogoro huo usifananishwe na tofauti za kisiasa kati ya CUF na CCM kwa kuwa sasa ni suala lililo kwenye jamii na kwamba Rais Magufuli anapaswa kuchagua maneno ya kuzungumza badala ya kutumia au kufikiria kwamba ubabe na hasira vinaweza kumsaidia.
Dk Bashiru alisema wapo watu wanaofikiria kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa suluhisho la hali ilivyo sasa lakini si kweli kwa sababu uchaguzi ni matokeo ya kuendeleza hali iliyopo na siyo kutafuta ufumbuzi.
Dk. Lwaitama
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Azaveli Lwaitama alisema anachofanya Rais Magufuli anajua faida na hasara zake, hivyo kuna uwezekano wa yeye kuangalia hali itakavyokuwa.
Dk Lwaitama alisema ni dhahiri kuwa Rais Magufuli amethibitisha kwamba uchaguzi ulikuwa halali, hivyo kutaka apeleke ujumbe kuwa mgogoro wa Zanzibar siyo uchaguzi.
“Kimsingi kauli hizo ni ngumu kuziunga mkono hasa sisi ambao tunatambua siasa za Zanzibar. Zinaweza kuzalisha jambo lingine ambalo halikuwepo, lakini tusubiri matokeo kama yatakuwa chanya au hasi,” alisema.
Lwaitama alisema marais wastaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa ndiyo wenye uwezo wa kutatua mgogoro wa Zanzibar.
Wanasiasa
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira alisema anaamini kinachohitajika Zanzibar si ubabe na kwamba kumlazimisha Rais Shein kuwa mkali si njia sahihi, kwani Wazanzibari wanatambua nini kilifanyika hata kufikia hali iliyopo sasa.
“Naamini Zanzibar kuna tatizo na kama tunahitaji kutatua njia ya mazungumzo ni muhimu zaidi kuliko ubabe na vitisho,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda alisema kauli za Rais ni za mrengo mkali ambao haujazoeleka nchini hivyo zinaweza kuongeza mgogoro.
Alisema kinachoonekana kwa sasa ni CCM kuendelea kupoteza nguvu Zanzibar, hivyo rais anapaswa kutumia diplomasia badala ya lugha ya ukali inayoweza kuvuruga mambo.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar (Chadema), Maraim Msabaha alisema kauli hizo zinawarudisha nyuma Wazanzibar kwani hali ilishaanza kutengamaa.
Msabaha alisema hadi sasa Pemba watu hawazikani, hawashirikiani katika sikukuu na mambo mengi ambayo ni ya kijamii, hivyo Rais angepaswa kusoma alama za nyakati na kuwa mstari wa mbele kumaliza mgogoro huo.
Mbunge wa Jimbo la Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky, alisema alichofanya Rais ni kutuma ujumbe kwa umma kuwa uchaguzi haupo, hivyo Wazanzibari wachape kazi.
Turky alisema kitendo cha Seif Sharif Hamad kukataa kumpa mkono Rais Dk. Shein mkono hakikupaswa kufumbiwa macho na alichofanya Magufuli ni sahihi.
0 comments:
Post a Comment