Videos

Sasa Wema amefuzu PhD ya mapenzi



JICHO LA TATU:


UMRI ni chuo. Unavyoishi unaona mengi na unaelemika katika vitu vingi. Kadiri binadamu wanavyoi­shi, ndivyo wanavyofanya makosa mengi. Wingi wa makosa huongeza uzoefu na mzoefu ni mwanazuoni.

Uanazuoni pia unatofautiana vi­wango. Kama ilivyo chuo kikuu kulivyo na shahada, uzamili na uzamivu, ndivyo na uzoefu ulivyo. Kama utafanikiwa kufumaniwa mara nyingi ndivyo na uanazuoni wako unavyokua, kutahamaki un­afikisha PhD ya kufumaniwa.Yaani wewe ni daktari wa falsafa za kufu­maniwa.

Unaweza kuwa na PhD lakini ukai­shia tu kuitwa daktari (dokta), lakini ukivuka viwango zaidi, unaitwa pro­fesa.Na profesa yeyote ni mwalimu wa kiwango cha juu katika taaluma yake chuo kikuu.

Umri ni elimu; Tendo moja la kipu­uzi likifanywa na watu wa aina tatu tofauti, tafsiri pia hutofautiana. Aki­fanya mtoto hupuuzwa kwa maneno “ni utoto, akikua ataacha”, ikiwa ni kijana husemwa “damu inachemka, ujana maji ya moto,” kwa mzee mwe­nye fainali yake kama isemwavyo fainali uzeeni, yeye husikitikiwa “mzee anazeeka vibaya.”

Maisha kila hatua kuna mitihani. Anayeishi miaka mingi kwa yakini anakuwa amekuwa amejaza majibu mengi. Kila hatua ina mafundisho, mitihani, majibu na ufaulu wake. Ukimuona mzee anafanya vituko, anafumaniwa au anajihusisha sana na mapenzi na vitoto, hapo kuna mawili, ama kuna mitihani aliruka au alikuwa anaibia majibu. Inaweze­kana pia alighushi matokeo.

Kawaida, mtu ambaye anaishi maisha yake umri huwa haudang­anyi. Atajidanganya kwa utoto wake, atakosea kwa ujana wake lakini ak­ishazeeka anakuwa mzoefu wa ku­jidanganya na utoto wake, vilevile anakuwa na majibu ya makosa ali­yofanya katika ujana wake, kwa hiyo hawezi kurudia makosa, maana ni mwanazuoni tayari.

Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu ni mwanazuoni sasa wa map­enzi. Jinsi anavyolia leo kukumbuka penzi la aliyekuwa boyfriend wake, marehemu Steven Kanumba, inato­sha kuonesha kuwa amepitia mengi ya kumfunza.

Mapenzi yana tabia ya kuwafanya watu wajute. Huwalazimisha wa­tenda makosa wajutie makosa yao wakati ambao muda umeshapita. Wenye kustahili kujuta, hujuta ka­tika nyakati ambazo haiwezekani kurudisha wakati nyuma. Wahenga walimaliza waliposema, majuto mjukuu!

Mfano leo hii Wema anamlilia Kanumba, atampata wapi? Mungu alishamchukua miaka minne iliyopita. Na hata wakati Kanumba anafikwa na mauti, hakuwa na Wema kimapenzi.

Kanumba na Wema wana visa vingi vya mapenzi. Nakumbuka kisanga cha Kanumba kuharibiwa gari na Wema. Siwezi kusahau pia kuwa Kanumba alimshtaki Wema polisi na kumsababishia alale mahabusu.

Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012, ilipofika Septemba 15, mwaka huu, Wema alichukua picha yake ya zamani aliyopiga na Kanumba, kweli ya zamani na muonekano wao wakiwa wadogo, Wema akaandika: “Pen­zi langu la kweli la kwanza. Wanasema una­pata penzi la kweli mara moja katika maisha.

“Kama ndivyo, vizuri siwezi kupingana na ukweli kuwa anayo nafasi muhimu kwenye moyo wangu. Baada ya Mungu kumchukua, nina chumba kingine kwa ajili ya mpenzi mwingine wa kweli. RIP Steve wangu.”

Maneno hayo ya Wema ndiyo yamenifanya niamini kuwa sasa amekua. Amepata uzoefu wa mapenzi. Kama mapenzi ni taaluma basi amekuwa mwanazuoni aliyekomaa. Ni kip­indi ambacho anayajua mapenzi ya kweli na udanganyifu wake. Na ndiyo sababu sasa an­amkumbuka Kanumba.

Siwezi kusema kweli Kanumba alimpenda sana Wema, maana Bongo Movie na mapenzi yao wanajuana wenyewe. Ila naweza kukiri kuwa Kanumba alihangaika mno kwa ajili ya Wema.

Alikuwepo muigizaji wa kike anaitwa Asha Jumbe.

Asha naye ana kaka yake anayeitwa Jumbe Yusuf. Mbele ya macho ya Kanumba, Wema akamtolea udenda Jumbe. Penzi lenye nguvu likachipua na kuchukua nafasi kubwa kati ya Wema na Jumbe.

Mama Wema, Mariam Sepetu, akaona mwanaye anapotea. Akalipiga vita penzi la Wema na Jumbe usiku na mchana.

Wema akajichimbia Tabata na Jumbe wake. Kanumba akawa anahangaika huku, mama Wema anarusha maneno kule. Wema haam­biwi hasikii kwa Jumbe.

Nakumbuka ilikuwa mwaka 2008, nikiwa mhariri wa gazeti moja la kila wiki, Wema alinipigia simu baada ya kuona kile ambacho mama Wema alikuwa am­ekisema na kuandikwa gazetini. Akasema naye anataka kufunguka.

Nilimwambia Wema nipo tayari kumsikiliza, akanielekeza Tabata alipokuwa anaishi, nami nikaon­doka na timu yangu tukamfua­ta. Tulimkuta Wema na Jumbe, alikuwepo pia Asha.

Wema alieleza jinsi alivyoanza uhusiano na Jumbe, akasema al­ipomuona tu alijikuta anavutiwa naye. Akasema yeye hampendi Ka­numba. Zikafuata tambo za Jumbe kuwa Kanumba hamuwezi na kwamba alishampiga walipo­kutana.

Maneno hayo ya Wema na Jumbe ndiyo yaliyoamsha hasira za Kanumba, akaen­da polisi kushinikiza Wema akamatwe kwa sababu aliharibu gari lake. Zilikuwa nyakati mbaya mno kwa watu waliopendana kufikia tamati ya aina hiyo.

Haina haja kugusia baada Wema kuachana na Jumbe alienda kwa nani na nani, ila nina stori ya mwaka 2011 Dodoma. Timu ya Bongo Movie ikiwa Dom, mimi pia nilikuwa kwenye shughuli zangu za uandishi. Kilikuwa kipindi cha vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kipindi hicho Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Plat­numz’ ametoka kutwaa tuzo tatu za Kili (KTMA), na wimbo unaotamba ni Mbagala, Wema tayari mpen­zi wa Diamond kwa wakati huo.

Nayakumbuka mazungumzo jinsi ambavyo Wema alikuwa akijaribu kuzungumza na Kanumba japo kawaida, Kanumba akawa anamjibu kuwa anaogopa kufanya mazungumzo na mke wa mtu kwa sababu hakuna asiyejua uhusiano uliopo kati ya Wema na Diamond.

Kanumba akaniuliza: “Eti Luqman, nani asiyejua kama sasa hivi Wema ni mke wa Diamaond? Wen­gine tuna damu mbaya, naweza kukaa pembeni na Wema, halafu ikasemwa mimi na Wema tumerudi­ana, mimi sitaki kabisa.”

Mimi hata sikuchangia neno, nilibaki najichek­elesha tu! Maana ningeweza kumuunga mkono Kanumba, kumbe alisema vile kwa sababu aliniona nipo karibu. Na ningemshauri Kanumba akubali ku­zungumza na Wema pembeni, Diamond angesikia si angekwenda kunikalia kikao Tandale? Sikutia neno kabisa.

Hata hivyo, baada ya kuona maneno hayo, na ni­kikumbuka sura ya Wema siku ile akimbembeleza Kanumba wazungumze, napata picha ni kwa kiasi gani mrembo huyo alimpenda godfather huyo wa Bongo Movie ambaye alikatika kama utani.

Kama Kanumba angekuwa hai, ningempigia simu na kumshauri akae chini na Wema wazungumze, la­kini haiwezekani. Siku zimepita na haziwezi kurudi nyuma. Nayaona maumivu ya Wema anapomkum­buka Kanumba wake.

Maneno ya Wema leo, yanaonesha jinsi ambavyo anatamani siku zirudi nyuma asimsaliti Kanumba kwa tamaa za kijana mwenye rasta Jumbe. Hata hivyo hayo hayawezekani tena. Hiki ndicho kipindi hasa ambacho Wema anaona makosa aliyofanya. Maana miaka imepita hamkumbuki Jumbe, anam­kumbuka Kanumba.

Wema katoka na wangapi wenye kujulikana? Ni wengi tu lakini kwa nini anamuwaza Kanumba kama mtu aliyekuwa na penzi la kweli kwake? Ni kwamba baada ya mitihani mingi, ameweza kueli­mika kwa kiwango cha kutosha.

Mitihani mingi ya kimapenzi, kutoka Kanumba kisha katikati kupita akina Jumbe, Charlz Baba, Dia­mond, Hartmann Mbilinyi, Idris Sultan na wengine ambao hajataka kuwaweka wazi, kwa hiyo sasa ame­kuwa mwanazuoni.

Maneno ya Wema kukiri kuwa Kanumba ndiye penzi lake la kweli la kwanza na kusema mtu huwa anapenda mara moja maishani, yanaonesha Wema tayari anamiliki shahada ya uzamivu (PhD) ya mizungu ya mapenzi.

Ni PhD ambayo inaweza sasa kumuongoza kuishi vizuri kimapenzi, maana ame­vuka mitihani mengi, kwa hiyo anayo majibu mengi kuhusu changamoto za mapenzi.

Wema anaweza kuwa mshauri kwa wengine, kwamba wakikutana na changamoto kama alizopi­tia wafanye nini ili kuvuka salama. Binafsi nimeanza kumwamini Wema kwa ua­nazuoni wake.

Ni shule pia kwa watu wengine wote kuwa wan­apokuwa na wapenzi wanaowapenda, watulie nao, dunia ina vishawishi vingi hii. Uaminifu ni kujizuia.

Ndimi Luqman Maloto
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment