MKAZI wa Lindi, Dennis Marcus na mkewe raia wa Uingereza, Antonia Martin, wamefunga ndoa kwa sherehe ya aina yake wakipanda bajaji na kunywa pombe ya kienyeji pamoja na wageni waalikwa.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Marcus alisema harusi hiyo ilifanyika Namanga, Lindi na waliamua iwe hivyo, ili kuonesha tofauti kati ya mila na utamaduni wa kiafrika na wa kizungu.
Alisema harusi hiyo ilifuata muda wa harusi za kawaida, lakini waalikwa walikula wali kwa maharage, pilau na kunywa pombe za kienyeji ili kuonesha utofauti huo.
“Nilitaka harusi iwe tofauti sana kwa kuwa kama ni gari lilikuwapo, hivyo haikuwa na haja ya sisi kulitumia, nikaamua kutumia bajaji kwa sababu si kitu kinachotumika katika harusi mara kwa mara,” alisema.
Mavazi
Kwa mujibu wa Marcus, gauni la harusi la mkewe lilishonwa nchini kwa ubunifu wake ingawa viatu, suti na ua la bibi harusi vilitoka Uingereza.
Akielezea historia yao, Marcus alisema walikutana na mkewe huyo mwaka 2008 Uingereza akiwa kwenye michezo ya sarakasi.
“Huwa nakwenda mara kwa mara Uingereza kwa masuala yangu na sarakasi na huko nilikutana naye,” alisema na kuongeza kuwa mkewe alisindikizwa na binamu yake na mtoto wake aliyezaa kabla ya wao kukutana.
“Mimi ndiye nilianza kumpenda ambapo mwaka 2008 nilikuwa nacheza ‘pool table’ ndipo akaja na rafiki yake nami nikamwambia jinsi ninavyojisikia,” alisema.
Alisema mwaka 2013 kulikuwa na mashindano ya sarakasi Uingereza ambapo mkewe alikuwa meneja na baadaye mwaka 2014 walikutana tena Dubai wakaendeleza mapenzi yao na Januari mwaka jana mkewe huyo alikuja nchini.
“Nahisi huyu ni mwanamke sahihi kwangu, pia kutokana na umri wangu kwenda, hivyo nahitaji mke wa kuishi naye kama vitabu vya dini vinavyosema,” alisema.
Marcus alisema aliona huyo mwanamke ndiye chaguo sahihi kwake na kuishi pamoja na kuzaa watoto na kujenga maisha ya baadaye.
Marcus alisema Julai 23 walifunga ndoa hiyo kwenye Kanisa Katoliki, Lindi na aliyewafungisha ndoa hiyo ni Padri Alkuine Innocent.
0 comments:
Post a Comment