MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema itaanza kutoa vitambulisho vipya vya Taifa vyenye saini kwa wananchi waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi na kuchukuliwa alama za kibiolojia.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew Massawe (pichani) uchukuaji wa vitambulisho hivyo utaanza kesho kwenye ofisi zote za Mamlaka hiyo zikiwamo za wilaya zilizoanza usajili Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Ruvuma na wabunge Dodoma.
Alisema waombaji wote ambao vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu zao kufahamishwa kufika kwenye vituo vya usajili kuvichukua.
“Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani visivyo na saini, ila kwa sasa vya zamani vitaendelea kutumika pamoja na vipya wakati taratibu za kuvibadilisha zikiendelea,” alisema.
Alisema kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji, ndiyo sababu vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika kwa huduma mbalimbali zinazohitaji kutambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.
Akizungumzia wananchi ambao hawakusajiliwa, Massawe alisema kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, waliwata kuendelea kujitokeza kusajiliwa kwani ni kazi endelevu.
Alikumbusha wananchi kutunza vizuri vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na kikipotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji alipie.
Alisema kwa sasa vitambulisho vya Taifa vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma nchini hususani kwenye benki kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupewa huduma, pia taratibu za kupanua wigo wa matumizi ya vitambulisho kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment