Videos

Kizimbani kwa kutishia kupindua Ikulu


Mshtakiwa Leonard Materu

MFANYABIASHARA Leornad Matelu (31), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa kutishia kupindua Ikulu kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Matelu alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Magreth Bankika wa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, akituhumiwa kuchapisha habari za uongo.

Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alidai kuwa Matelu ambaye ni mkazi wa Moshi Baa kwa Diwani, Mombasa, Dar es Salaam, anatuhumiwa kuchapisha habari za uongo kwa njia ya mtandao.

Ilidaiwa kuwa Julai 17, Matelu akiwa Dar es Salaam alichapisha ujumbe wenye lengo la kuudanganya umma kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Lukondo alidai kupitia mtandao huo kuwa: “Magu ajiandae tunakwenda kupindua hadi Ikulu,” maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais John Magufuli.

Baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka, alikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo Lukondo alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Pia alidai kuhusu dhamana ya mshitakiwa huyo hana pingamizi kwa sababu mashitaka yanayomkabili kisheria yanadhaminika.

Wakili wa Matelu, Neema Lamwai aliomba dhamana ya mteja wake kwa sababu sheria iko wazi kuwa mashitaka hayo yana dhamana.

Mshitakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana, na kesi hiyo itatajwa Septemba 20.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment