Videos

Tume ya Uchaguzi yafikiria vitambulisho vya Taifa


Jaji Damian Lubuva
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafikiria kuanza kutumia vitambulisho vya Taifa kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika hivi karibuni Botswana.

Jaji Lubuva alisema katika mkutano huo ambao alifuatana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, walijifunza mambo mengi ambayo wanaweza kuyatumia kwenye uchaguzi ujao kulingana na sheria za nchi likiwamo suala la kutumia vitambulisho hivyo na kuachana na vya mpiga kura.

“Katika mkutano ule tulijifunza mengi ambayo tungeweza kuyatumia kuboresha uchaguzi wetu lakini kwa sasa ambalo naweza kusema tuliangalie ni kutumia kitambulisho cha Taifa kama kadi ya mpiga kura lakini hili litatarajia pia na sheria zetu,’’ alisema Jaji Lubuva.

Alisema katika nchi zinazotumia vitambulisho hivyo, sheria zao zinawataka kufanya hivyo tofauti na nchini ambapo sheria inataka kutumia kadi ya mpiga kura.

Alisema katika uchaguzi ujao endapo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) itakuwa imekamilisha kuandikisha wananchi wote na kuwapa vitambulisho, NEC itaangalia sheria ilivyo na kushauri namna ya kuifanyia marekebisho.

“Kuna baadhi ya mambo ambayo tuliona kwa wenzetu ambayo yanafaa kuigwa na ni mazuri, kwa mfano hilo la kutumia kitambulisho cha Taifa,” Jaji Lubuva alisema.

Suala lingine lilihusu kuruhusu Watanzania walio nje ya nchi ambapo alisema ili kulifanyia uamuzi mzuri ni vema likapelekwa taratibu na kuangalia faida na athari zake.

Alisema katika mkutano huo baadhi ya wajumbe wa tume za nchi wanachama ambao walikuja nchini kuona uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, walipongeza namna uchaguzi huo ulivyofanyika kwa uhuru na uwazi na pamoja na ushindani mkubwa, ulimalizika salama.

“Moja ya mambo ambayo wenzetu pia walijifunza kwetu ni jinsi tulivyoandikisha idadi kubwa kwa miezi michache, huku kukiwa hakuna vifaa vya kutosha na jinsi uchaguzi wetu ulivyokuwa na ushindani lakini tukatoka salama,’’ alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment