Videos

Wahariri wapinga Serikali kufunga redio



Suleiman Msuya

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limepinga uamuzi wa Serikali kuvifunga vituo Radio 5 ya Arusha na Magic FM cha Dar es Salaam likieleza kuwa uamuzi huo haukuzingatia misingi ya utawala bora na kutoa mwito kwa Waziri husika kutafakari upya suala hilo.

Taarifa iliyotolewa jana na TEF kupitia Katibu Mkuu wake, Neville Meena, ilisema kwa  miezi takriban 10 tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye, amejitokeza mara nne kutangaza kufuta na kufunga baadhi ya vyombo kwa muda usiojulikana.

Alisema TEF imeshitushwa na kusononeshwa na hatua ya Serikali kupitia kwa Waziri huyo kuvifunga kwa muda usiojulikana vituo hivyo, huku sababu iliyotolewa ikiwa ni siri yake.

TEF ilisema kwa sababu hiyo, si rahisi kwa waandishi wengine wa habari kujifunza kwa makosa ya wenzao kwa kuwa mchakato uliotumika kushughulikia suala hilo umebaki kuwa siri ya Waziri.

“Alianza kulifuta Gazeti la Mawio, baadaye alitangaza kufuta mamia ya magazeti na majarida ambayo hayajachapishwa kwa muda mrefu, ikafuata adhabu ya kulifungia kwa miaka mitatu Gazeti la Mseto na sasa vituo viwili vya redio,” alisema.

Alisema katika tukio la kufutwa kwa Mawio, walihoji ukubwa wa kosa la gazeti hilo na sababu za kufutwa. “Leo hii tunahoji tena ukubwa wa makosa na pengine historia ya redio husika siku zilizopita. Ndiyo maana tunasema hili la sasa ni mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa habari,” taarifa hiyo ilisema.

TEF ilisema inachukulia hatua hiyo kama mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini na wanashindwa kuelewa dhamira ya Serikali kwa sekta ya habari nchini.

Ilisema kinachoonekana ni kutumia kila aina ya sheria  kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kuwa hawaoni nia ya malezi katika uamuzi wa Waziri.

Msimamo wa TEF

Utaratibu uliotumiwa na Waziri hata kufikia uamuzi huo, umekuwa wa makosa ya siku zote. Pamoja na kwamba vyombo vya habari hufanya makosa, lakini hata makosa yanapotokea taratibu za kuyashughulikia lazima zizingatie misingi ya utawala bora, haki na demokrasia.

Mfumo wa kushughulikia matatizo au kasoro za kitaaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwani unamfanya Waziri kuwa na mamlaka ya kutoa adhabu, kwa kuzingatia mtazamo wake, hata kama unakinzana na misingi ya taaluma.

Kimsingi uamuzi wa Nape unaonekana kukosa nia njema ndani yake, kwani Kifungu cha 28 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alichotumia kutoa adhabu hiyo, hakimlazimishi kufungia vituo vya redio kama alivyofanya.

Kosa la vituo hivyo kwa mujibu wa Waziri ni uchochezi, lakini hakuweka bayana maudhui ya vipindi au habari ambazo zilivifanya vituo hivyo ‘kutiwa hatiani’ na baadaye kufungwa kwake kwa muda usiojulikana.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment