Mwandishi Wetu
BARAZA Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), linatarajia kukutana siku chache zijazo kujadili pamoja na mambo mengine, hatima ya uanachama wa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake.
Wengine ambao wanatarajiwa kujadiliwa uanachama wao ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya, Mbunge wa Mtwara Mjini Maftah Machuma, Thomas Malima, Ashura Mustapha na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya na wengine wengi.
Taarifa ambazo JAMBO LEO ilizipata kutoka chanzo cha uhakika ndani ya CUF, zilisema maandalizi ya vikao vya wazee ambao watajadili sakata hilo ambalo linaweza kusababishamigogoro ndani ya chama yanaendelea.
Mtoa habari huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema wamekusanya ushahidi wa kutosha kuhusika kwa watu wa CCM,hivyo wanatarajia kufanya uamuzi mgumu ambao utakiacha chama kikiwa salama.
“Sisi tumepata ushahidi wote kuiwa watu wa CCM wanatuma fedha kwa mitandao ya simu kwa watu wetu, hivyo tumeamua kuwapa nafasi wazee ili wapitie hatua kwa hatua na tutaitisha Baraza Kuu Maalumu, ili kufanya uamuzi,” alisema.
Mtoa habari huyo alisema utaratibu anaoutumia Profesa Lipumba haukubaliki kwani lengo lake ni kuvuruga chama huku akisisitiza kuwa CUF inaweza kuendelea kuwa imara bila yeye.
Alisema Profesa Lipumba amediriki kumwambia Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kuwa atahakikisha anarejea CUF kwa njia yoyote la sivyo chama kife.
“Hakuna sababu ya kubaki na mnafiki anajaribu kutupotezea muda, aliondoka katika kipindi kigumu na akasema anakwenda kufanya uchambuzi wa uchumi, sasa anataka kurudi kwa fujo haikubaliki,” alisisitiza.
Alisema ushahidi wa CUF kupata mafanikio upo kwani aliondoka wakiwa na wabunge wawili wa kuchaguliwa na sasa ni 10 na inaongoza baadhi ya majiji na halimashauri. Profesa Lipumba alijiondoa kwenye wadhifa wa uenyekiti wa chama hicho mwaka jana akipinga kupokewa kundini (UKAWA) kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na kusimamishwa kugombea urais kwa tiketi ya Chadema kuungwa mkono pia na Ukawa.
Hata hivyo, alibwagwa na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ambaye hivi sasa ni Rais wa Awamu ya Tano.
Baada ya kushindwa, hivi sasa Lowassa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na anaongoza Operesheni Ukuta kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Hivi karibuni, Profesa Lipumba alibadili mawazo na kuomba kurejea ulingoni akitaka kugombea uenyekiti wa chama hicho, hatua ambayo imesababisha mgawanyiko ndani ya chama hicho, hata kuvuruga Mkutano Mkuu maalumu uliofanyika juzi Dar es Salaam.
Maalim lawamani
Naye Emeresiana Athanas anaripoti kwamba, siku moja baada ya Mkutano Mkuu wa CUF, kuvunjika kutokana na mvurugano uliotokea baadhi ya wanachama wamedai kilichotokea ni mipango ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kukivuruga.
Taarifa za ndani ya chama hicho zilieleza kuwa hadi sasa wanachama zaidi ya 300 wakiwamo wajumbe wa Kamati Kuu wamejitokeza kupinga matokeo ya upigaji kura wa kukubali au kukataa kujiuzulu kwa Profesa Lipumba ndani ya CUF.
Mvurugano huo ulitokea juzi katika ukumbi wa Blue Pearl Ubungo kwenye mkutano huo wa dharura kwa ajili ya kupokea taarifa na kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho zilizoachwa wazi.
Walitoa madai hayo Dar es Salaam jana, wakati wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wakidai mkutano huo haukufanyika kihalali kutokana na sehemu ya wanachama zaidi ya 100 kuingia kinyume na utaratibu.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na chama hicho kupitia Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani ilisema pamoja na kuahirishwa kwa mkutano huo kutokana na vurugu kitatoa taarifa ya marudio ya mkutano kwa ajili ya kuziba nafasi zilizo wazi.
0 comments:
Post a Comment