Videos

Serikali yafunga vituo vya redio



Leonce Zimbandu

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amevifunga kwa muda vituo vya Radio 5 cha Arusha na Magic FM cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, hatua hiyo imefikiwa baada ya kujiridhisha  kuwa kipindi cha Matukio kilichorushwa Agosti 25,  saa 2 usiku na Radio 5 na cha Kupaka Rangi kilichorushwa Agosti 17, na Magic FM  vilikuwa na maudhui ya  uchochezi.

Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana kwa kusisitiza vipindi hivyo kuwa na maudhui ya uchochezi ambao ungeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema vitendo vilivyofanywa na vituo hivyo vinakiuka kanuni ya 5 (a),(b),(c) na d, pia kanuni ya 6(2), (b),(c) na 18  (1), b(i),(ii) na (iii) ya huduma za utangazaji na maudhui ya mwaka 2005.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 28 (1) cha sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mwaka 2003 ninavifunga vituo hivyo hadi Kamati ya Maudhui itakapoviita vyombo hivyo kuvisikiliza,” alisema.

Alisema baada ya Kamati kusikiliza vyombo hivyo, itatoa mapendekezo ya kumshauri Waziri hatua zinazopaswa kuchukuliwa, lakini kwa sasa hatua iliyochukuliwa itakuwa ya muda.

Aidha, Waziri Nape alipongeza vyombo vingine vya habari vilivyojikita kutekeleza wajibu wao wa sheria, kanuni na kufuata weledi wa tasnia ya habari katika kuleta amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya nchi.

Alisema Serikali inaendelea kuvihadharisha vyombo vya habari kutoshawishika kuvunja sheria na kanuni zinazoongoza tasnia ya habari ili kulinda heshima ya tasnia na amani ya nchi.

Vyombo hivi vimefungwa huku gazeti la Mawio nalo likiwa kifungoni kwa tuhuma za uchochezi.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment