Videos

'Chanzo cha Richmond uchu wa madaraka'



Edward Lowassa

ALIYEKUWA Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, ametaja mambo matatu ambayo hatayasahau katika utumishi wake bungeni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Jambo Leo Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Joel alitaja mambo hayo kuwa ni sakata la Richmond, Escrow na G55, akieleza kwamba yaliibuliwa kwa sababu za kutafuta madaraka.

Alisema katika maisha yake ya utumishi hatasahau sakata la Richmond lililomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa ajiuzulu. Hata hivyo, alisema kama Bunge la kipindi hicho mwaka 2008 lingejikita katika kufanya uchunguzi wa kina, huenda yaliyotokea, yasingetokea.

"Hapakuwa na uchunguzi wa kina juu ya masuala hayo," alisema Joel ambaye sasa amestaafu baada ya kuhudumu katika ofisi ya Bunge kwa miaka 24.

Katibu huyo wa Bunge wa zamani, ambaye alianza kazi enzi za Bunge la chama kimoja, alisema ataendelea kulikumbuka kundi la G55 kwa hatua yake ya kutaka kudai uwepo wa Tanganyika, akisema bila marehemu Mwalimu Julius Nyerere kuingilia kati, sakata ilo lingeing’oa Serikali na kuvunja Muungano.

Joel alisema katika utumishi wake bungeni tukio la Richmond alilifananisha na sakata la Escrow na kueleza kwamba ilikuwa ni vita ya madaraka.

Alisema kwa kuanzia na sakata la Richmond ambalo lilimfanya Lowasa kuwajibika kwa kijihuzulu mwaka 2008, sakata ilo halikufanyiwa uchunguzi wa kina na badala yake lilimalizwa kwa woga.

“Kwa mfano sakata la Richmond, ilibidi aliyekuwa Waziri Mkuu awajibike, lakini ukilichunguza kwa undani kabisa, utaona halikuwa limefanyiwa utafiti wa kutosha, lilitufikisha tulipofika sababu ya woga," alisema Joel.

Alisema kupitia sakata hilo, pande mbili zilizokuwa bungeni, zililibeba kwa sura mbili tofauti huku akifafanua kuwa CCM walilibeba kwa woga na kuona kuwa wasingelipatia ufumbuzi lingeweza kuiangusha Serikali, huku wapinzani wakilichukulia kwa sura ya hoja ya kuingilia madaraka.

Aliongeza kuwa sakata hilo halikuwa limefanyiwa uchunguzi wa kina kwa kuangalia chimbuko la tatizo, na badala yake wahusika walijikita zaidi kwa kutazama mtu na kwamba ungekuwapo ufuatiliaji mzuri yasingetokea yaliyotokea ambayo alidai yalileta uadui pia.

"CCM waliona pesa nyingi zimetumika, kwa hiyo wakaona wasipolibeba wao Serikali ingeweza kuanguka, lakini kwa Upinzani nao walitaka kulibeba kwa sura ya kuona kama wangeweza kutumia hoja hiyo kuingia madarakani.

"Lile suala lingekuwa limefanyia uchambuzi wa kina kwa kuangalia tatizo lilipo, halafu lifanyiwe kazi tatizo badala ya kujihusisha na watu, pengine tusingefika tulikofika na pengine tusingefikia hali ya kuwa na uadui ambao ulijitokeza.

"Kulikuwa na haja ya kufanywa uchunguzi wa kina, wangekwenda kushughulika na hayo, badala ya watu na madaraka," alisema Joel. Sakata la Richmond lilihusu ufisadi uliotokana na uagizaji wa mitambo ya kufua umeme ili kukabiliana na tatizo la umeme lililoikumba nchi wakati huo.

Akioanisha sakata hilo na la Escrow lililoibuliwa bungeni siku za karibuni, Joel alisema matukio hayo yanafanana na yakitazamwa kwa kina bado yanahusu madaraka na si zaidi ya hapo.

Saka la Escrow lilitokana na ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta Escrow ulioombwa na Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini ufanywe na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ukaguzi huo ulilenga kufanya uchunguzi wa kina aili kutoa taarifa kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala kwenye akaunti maalumu ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa.

"Sakata la Richmond ni sawa na Escrow, nakumbuka tulifanya kazi tangu saa tatu asubuhi mpaka saa nane usiku, lakini ukiangalia kwa undani ni madarakaÖni madaraka tu hakuna kitu kingine," alisema.

Aliongeza kuwa suala la madaraka liligusa CCM na Upinzani, na ndiyo maana sakata hilo liliibuliwa kipindi cha mwelekeo wa Uchaguzi. Escrow iliingia wakati wa kipindi cha kuelekea uchaguzi, ilikuwa ni kutafuta nani anaingia madarakani kila upande ukitaka kutazama nani anabaki nani anangíoka," alisema.

"Escrow ilikuja kama njia ya kutafuta madaraka, Upinzani waliitumia baada ya kushindwa kwenye Richmond, na ukiangalia uanzishwaji wa Escrow upo kisheria, lakini ikaingizwa ndani ya Bunge kama ajenda ya kisiasa, lengo kubwa Serikali ianguke, vivyo hivyo kwa CCM ilikuwa Fulani asichukue madaraka, Fulani aachwe," alisema Joel.

Kundi la G55 Kuhusu sakata la kutaka kuvunjwa kwa Muungano kwa kudaiwa kwa Tanganyika liloibuliwa na kundi la wabunge 55 mwaka 1993 likiitwa G55, Joel alisema hatasahau sakata hilo, kwa kuwa lilitikisa nchi na Serikali.

Alisema kundi ilo la wabunge lilokuwa likiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lupa Njelu Kasaka (CCM), lilitikisa kwa kuwa lilikuja bungeni na hoja nzito iliyogusa mustakabali wa nchi.

Kundi hilo lilitaka Muungano upitiwe upya na ikiwezekana uboreshe na kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika. Joel alisema hatalisahau na kufafanua kuwa kwa mara ya kwanza alimshuhudia Mwalimu Nyerere akilazimika kuingia bungeni kutafuta suluhu.

"Kundi lile la G55 lilitikisa nchi, liliyumbisha nchi sababu ilikuwa inahusu Muungano, lakini ilikuwa ni kwa ajili ya kujenga misingi iliyo imara. "Kama si Nyerere, nadhani Muungano usingekuwapo tena, sababu tulifika pabaya sana, suala hilo lilipatiwa suluhu baada ya kukubali kutokubaliana na Mwalimu Nyerere alilazimika kuingilia kati," alisema Joel.

Mbali na Kasaka wengine waliounda kundi hilo ni Lumuli Kasupa (Kyela), William Mpiluka (Mufindi), Mateo Qaresi (Babati), Jared Gachocha (Ngara), Tito ole Kipuyo (Arusha), Philipo Marmo (Mbulu), Arcado Ntagazwa (Muhambwe) na Patric Qorro (Karatu).

Wengine ni Japhet Sichona(Mbozi), Jenerali Ulimwengu (Taifa), Abel Mwanga (Musoma Mjini), Profesa Aaron Massawe (Moshi Vijijini), Shashu Lugeye (Solwa), Sebastian Kinyondo (Bukoba Vijijini), Phares Kabuye (Biharamulo Magharibi) na Mbwete Hombee (Rungwe). Pia Kisyeri Chambiri (Tarime), John Byeitima(Karagwe), Abdalah Nakuwa (Lindi), Ndembwela Ngunangwa(Njombe Kusini), Mathias Kihaule (Ludewa), Mussa Nkhangaa (Iramba), Edward Ayira (Rorya), Adam Karumbeta (Mbeya) na Halimeshi Mayonga (Kigoma Vijijini).

Wabunge wengine ni Dk John Katunzi (Geita), Ismail Iwvata (Manyoni Magharibi), Tobi Mweri (Tanga), Aidan Livigha (Morogoro), Tabitha Siwale(Taifa), Obel Mwamfupe (Mbeya), Othman Mpakani, Evarist Mwanansao (Nkasi) na Paschal Degera (Kondoa Kaskazini).

Hali kadhalika Erasto Losioki (Ngorongoro), Nasoro Malocho (Mtwara), Charles Kagonji (Mlalo), Venance Ngula (Taifa), Benedicto Lusurutia (Kiteto), Dk Deogratius Mwita (Serengeti Pius Nko (Arumeru), J. Mwanga na Chadiel Mgonja (Same), Pia walikuwamo Guntram Itatiro (Ifakara), Paschal Mabiti (Mwanza), Edith Munuo (Taifa), Raphael Shempemba (Lushoto), John Mhina (Muheza), George Nhigula (Kwimba), Kapteni Thadeus Kasapira (Ulanga Magharibi), Charles Kinuno (Nyangíhwale), Christian Fundisha (Tabora Kusini), Samwel Rwangisa (Bukoba Mjini) na Maria Kamm (Taifa).
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment