Na John Banda, Dodoma
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi ya Wasioona Buigiri Misheni iliyoko katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wamemwomba diwani wa kata hiyo Keneth Yindi greda la kusawazisha maeneo ya shuleni hapo ambayo yamekuwa na mashimo na mifereji iliyokuwa ikipitisha maji katika kipindi cha cha mvua.
Ombi hilo limetolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shuleni hapo,baada ya kujionea jinsi wanafunzi wasioona walivyokuwa wakitembea kwa tahadhari kubwa kutokana na hofu ya kutumbukia kwenye mashimo na mifereji hiyo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Mariam John anayesoma darasa la sita mwenye uoni hafifu, alisema kuwa hivi sasa wanafunzi wamekuwa wakianguka hovyo kwa kujikwaa na wengine kutumbukia kwenye mifereji iliyokuwa ikipitisha maji.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo wanamwomba diwani huyo greda kwa ajili ya kusawazisha maeneo hayo ya shule ili wanafunzi waweze kutembea bila hofu ya kujikwaa na hatimaye wengine kuanguka.
Alisema hivi sasa kutokana na kuwepo kwa mashimo na mifereji hiyo, wanafunzi hao wamekuwa wakitembea kwa tahadhari kwa kuhofu kuumia licha ya kupewa msaada na wezao ambao wanaoona.
“Kwa kweli sisi wanafunzi tunamwomba diwani wetu atutupie jicho la huruma ili turekebishiwe maeneo haya ya shule ambayo karibu sehemu nyingi kuna mifereji na mashimo yanayotufanya tuwe tunajikwaa kwa s ababu ya kutoona kwetu,” alisema..
Hata hivyo, wanafunzi hao walisema pamoja na changamoto hiyo,pia wanakabiliana na uchakavu wa samani ya vifaa vya shule kama vile viti na meza, huku kwa wale wanaotumia mashine ya nukta nundu wakichangia zaidi ya watatu hadi wanne kwenye mashine moja.
Mwanafunzi Atanance Mathayo anayesoma darasa la tano alisema kuwa wanapeleka maombi hayo kwa diwani huyo kutokana na umuhimu aliokuwanao wa kuchangia watu wenye mahitaji mbalimbali. Alisema kuwa wao kuwa wanafunzi ni matumaini yao diwani huyo anaweza kuwasaidia kama anavyoweza kutoa misaada mingine kwa watu wengine.
0 comments:
Post a Comment