Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara imemwamuru Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi, kujieleza kwa nini asifungwe jela kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya kulipa dola 598,750 za Marekani sawa na Sh bilioni 1.2.
Kiwango hicho ni malipo ya wafanyabiashara watatu; Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles Mgweo, kutokana na mgogoro unaohusu malipo ya uuzaji hisa kwenye kampuni ya Douglas Lake Minerals Ltd, ambayo kwa sasa inaitwa Handeni Gold Inc.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na wafanyabiashara hao ilisikilizwa na Jaji Agathon Nchimbi huku Dk Mengi na kampuni ya K.M. Prospecting Limited wakiwa ndio walalamikiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mwito, Dk Mengi anatakiwa kufika mahakamani hapo Agosti 24 kujieleza kwa nini asifungwe gerezani kama sehemu ya kukazia hukumu hiyo.
Hatua hiyo ya Mahakama inatokana na wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi ya kuiomba Mahakama ikazie hukumu hiyo ya Januari 28.
Hati ya kiapo cha pamoja cha wafanyabiashara hao, ilieleza kuwa walifungua shauri kwenye Mahakama hiyo wakidai malipo yaliyobaki ambayo ni dola 428,750, dola 100,000 na dola 70,000, kila mmoja.
Walieleza kuwa baada ya ushahidi kutolewa, Mahakama ilitoa hukumu dhidi ya walalamikiwa na hadi jana hawakuwa wamekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Walisema ingawa Dk Mengi ni mfanyabiashara maarufu anayejulikana kuwa na fedha, akaunti za benki, mali zinazohamishika na zisizohamishika, lakini juhudi za wao kupata mali hizo zikiwa na jina lake au ushahidi wowote wa umiliki wake, ziligonga mwamba.
Walalamikiwa wameeleza kuwa juhudi kama hizo zimefanyika pia na Kampuni ya K.M. Prospecting Limited ambayo pia inadaiwa, lakini zimeshidikana kuwa mali na akunti zake za benki hazijulikani zilipo.
Kufuatia hali hiyo, walalamkaji wanaeleza kuwa juhudi za kukamata mali za walalamikiwa ili kutimiza matakwa ya hukumu iliyotolewa yameshindikana.
Hivyo walidai kuwa namna pekee ya kutekeleza hukumu hiyo ni kumtaka mlalamikiwa afike mahakamani na kujieleza kwa nini asipelekwe gerezani na kwamba ni jukumu lake kueleza mali zake ziliko ili zitumike kutekeleza matakwa ya hukumu.
Taarifa zaidi zilionesha kuwa tayari Dk Mengi alishapelekewa hati ya mwito huo wa Mahakama.
0 comments:
Post a Comment