Videos

Lowassa sasa atuma waraka Polisi, CCM



Suleiman Msuya

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ametoa waraka akieleza alichokiita masikitiko yake kwa jinsi Serikali inavyoelekea kulitumbukiza Taifa kwenye mkwamo.

Katika waraka huo alioutuma jana kwa vyombo vya habari kupitia Msemaji wake, Abubakar Liongo, Lowassa alisisitiza kwamba maandamano ya Ukuta yatakayofanyika kesho yatakuwa ya amani.

“Tumelazimika kutangaza Operesheni Ukuta kupinga ukandamizaji huo. Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi Watanzania walivyoipokea Operesheni hii licha ya vitisho vya Dola,” alisema Lowassa.

Kwa mujibu wake, kukutana kwake na Rais John Magufuli na kusalimiana katika Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kulikuwa ni mwanzo wa juhudi za kuondoa sintofahamu iliyokuwapo.

Lakini akasema kitendo cha juzi yeye na viongozi wenzake wa Chadema kukamatwa na Polisi, kimerudisha nyuma juhudi hizo.

“Cha kushangaza wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo. Jana (juzi) tukiwa kwenye kikao cha kujadiliana jinsi ya kuunyosha zaidi mkono huo, Jeshi la Polisi likaja na kuukata kwa kutukamata,” ilieleza sehemu ya waraka huo.  

Lowassa alisema anasikitishwa na utaratibu wa Polisi kunyanyasa na kusumbua viongozi na wanachama wa   Upinzani hasa Chadema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema amepokea simu nyingi kutoka kwa viongozi wastaafu na watu wengine mashuhuri na wa heshima kubwa nchini kuwataka wazungumze na Serikali ili kuepusha Taifa kutumbukia kwenye machafuko.

Alisema kitendo hicho kwake binafsi kimezidi kumwimarisha na kumpa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu Katiba, ambayo viongozi  waliapa kuifuata na kuitetea.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema amelazimika kushika kalamu na kuandika masikitiko yake, kwa jinsi Serikali ya CCM inavyoelekea kulitumbukiza Taifa  kwenye mkwamo na machafuko ya kisiasa.

Sote tunafahamu hali ya kisiasa ilivyo tete kwa sasa nchini. Serikali inaukandimiza Upinzani na demokrasia kwa jumla. Tumelazimika kutangaza Operesheni Ukuta kupinga ukandamizaji huo,” alisema.
 
Alisema siku zote Chadema na Ukawa wanalitakia  amani na utulivu Taifa la Tanzania, lakini vitendo vya   Polisi vimewapa wasiwasi Watanzania.

Kwa takriban mwezi mmoja sasa kuna hali ya sintofahamu kati ya Polisi, Serikali na vyama vya siasa baada ya Jeshi hilo na Rais Magufuli kutangaza kuzuia mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020 na kutaka  ifanywe na wabunge katika majimbo yao tu.

Kauli hiyo ilisababisha mijadala kupitia mitandao ya kijamii na vyama vya siasa, hata kuzaliwa Ukuta ambao unarajia kufanya mikutano na maandamano kuanzia kesho nchini kote kwa kinachodaiwa ni kupinga ukandamizaji wa demokrasia na udikteta.

Tangu Ukuta utangazwe, habari katika kila kona ya nchi imekuwa ni Ukuta hali ambayo imesababisha kuwapo kwa taharuki huku kila upande ukitunisha misuli na kukosekana kwa majadiliano ya kutatua.

Mvutano huo ulipelekea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Msajili wa Vyama Siasa, viongozi wa dini wanasiasa maarufu na makundi   kujitokeza mbele ya vyombo vya habari na kukemea na kuomba mazungumzo yafanyike, ili kutoingiza nchi kwenye machafuko.

Wakati jitihada hizo zikifanyika, juzi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alijitokeza akasema kuwa tamko la Polisi halijadiliwi kwa sababu ni la kisheria na kikatiba na kuwa masuala ya kisiasa yanapaswa yajadiliwe katika Baraza la Vyama vya Siasa.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment