Saed Kubenea |
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amefikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya saa 2, kutokana na tuhuma za kuandika makala ya uchochezi kwenye gazeti la Mwana Halisi Julai 25 na 31.
Aidha, Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruku (CUF) aliyekamatwa juzi saa nne asubuhi kwa madai ya uchochezi alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, baada ya Kubenea kuhojiwa, Wakili wake, Tundu Lissu alisema Polisi ilimwita kwa mahojiano kuhusu makala hayo yaliyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu Zanzibar, ambapo kwa mujibu wa Jeshi hilo, ni ya kichochezi.
Alisema katika mahojiano hayo Kubenea alitakiwa kuelezea watu aliodai waliteswa kama alionana nao na kuwasiliana na Polisi na kwamba asilimia kubwa ya maswali hayo yalihusu makala hiyo.
Alisema Kubenea aliachiwa kwa dhamana ya Polisi na kutakiwa kuripoti Agosti 18, kwa hatua nyingine za kipolisi. Wakili alisema jitihada zinazofanywa na Serikali na Jeshi hilo ni kuwanyamazisha lakini hazitafanikiwa kwani dhamira yao ni kupigania haki, sheria na kulinda Katiba ya nchi na si vinginevyo.
Naye Ibrahim Kunoga anaripoti kutoka Tanga, kwamba Polisi wilaya ya Tanga, imemwachia kwa dhamana ya Sh milioni 20 Mbunge Mbaruku aliyekamatwa kwa madai ya kufanya mikutano ya hadhara na kutoa maneno ya uchochezi na yanayoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupewa dhamana, Mbunge huyo alisema kilichofanywa na Polisi ni mwendelezo wa uminyaji haki ya demokrasia ili viongozi wakose uhuru wa kuzungumza na wananchi.
Mbaruku alisema Jeshi hilo lilimtaka asiendelee na mikutano ya hadhara, asitoke nje ya Tanga na kuzuiwa hati yake ya kusafiria. Alisema CUF itaendeleea kupinga hatua hiyo ya Polisi ili kufikisha ujumbe kwa wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
Mwenyekiti CUF wa Wilaya, Rashid Jumbe alilaani kitendo cha Jeshi hilo kumkamata mbunge huyo ambaye alikuwa akitekeleza majukumu ya kawaida ya kichama na kufikisha ujumbe kwa wananchi wake.
Jumbe alisema wataendelea kumwunga mkono ili kuhakikisha haki inatendeka na kuwataka wananchi wa Tanga pia kumwunga mkono pamoja na chama ili kufikisha dhamira nzuri ya kutekeleza majukumu ya kichama.
0 comments:
Post a Comment