Videos

Msekwa: Lowassa hakukosea kuhama

*Asema hatahivyo nguvu zilibaki CCM
* Ni sawa na alivyoondoka Mrema

Moi Dodo

SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amesema Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa hakukosea kuondoka CCM na kujiunga na upinzani, lakini asijidanganye kuwa bado ana nguvu kisiasa.

Msekwa alisema hayo hivi karibuni alipozungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

“Kwenye Biblia kuna mtu anaitwa Samson alikuwa na nguvu nyingi, aliweza kuvunja hata mageti ya chuma. Maadau zake walipoona wamemshindwa wakaamua kumtumia mwanamke sijui anaitwa nani yule…”

Aliendelea “yule mwanamke alimdanganya na akafanikiwa kumwambia kuwa nguvu zake ni nywele zake na walipomnyoa kweli bwana nguvu zake zikaisha.”

“Sasa Lowassa asijidanganye kuwa bado ana nguvu kisiasa, ni kama Samson. Yeye alipotoka CCM akaacha nguvu zake huko. Nywele za Lowassa na hata Mrema wakati huo ni CCM. CCM ina nguvu ya asili ambayo mtu ukitoka unaiacha.” 

Majibu wa Lowassa

Alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Msekwa, Lowassa alisema “Hayo ni maoni yake, hivyo hawezi kuyajadili.”

Alisema “Msekwa alisema lini hayo? Lakini siwezi kuzungumzia hilo kwa kuwa hayo ni maoni yake na nguvu zangu Msekwa hawezi kuzijua.”
Kwa nini hakukosea kuhama?

“Wale wanaodai kuwa alifanya kosa, wanaudanganya umma. Hakukosea kabisa. Ukisoma Katiba ya CCM, kifungu cha 13, kinaeleza kuwa mtu anaruhusiwa kujitoa ndani ya chama kwa kujiuzulu au kuhamia chama kingine, endapo ataona kuwa utendaji wa chama haumridhishi.

“Kwa hiyo, Lowassa aliona kuwa haridhishwi na mambo yanavyoendelea ndani ya CCM ndiyo maana akaamua kuondoka na kuhamia Chadema ambako aliona kunamfaa zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza;

“Katiba ya chama iko wazi na wala haimfungi mwanachama kuhama au kujiuzulu. Ukiona kuwa mambo yanayotendeka ndani ya chama hayakuridhishi, basi uko huru kuondoka na wala hakuna atakayekuuliza.”

Mtikisiko wa Lowassa

Akizungumzia mtikisiko uliosababishwa na kuondoka kwa mwanasiasa huyo nguli, Msekwa alisema CCM haikupata wakati mgumu, kwani ina nguvu kubwa ambayo inaifanya ipambane nyakati zote.
“CCM haikitikiswa kwa namna yoyote na kuondoka kwa Lowassa, kwani ilishajiandaa na ikumbukwe kuwa chama kina nguvu ya ndani ambayo inakifanya kihimili vishindo vya kila namna. Hivyo watu waache kuamini kuwa kuondoka kwa Lowassa kuliifanya CCM ipitie wakati mgumu kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Msekwa.

Msekwa alisema kuondoka kwa Lowassa ndani ya CCM kunafanana kwa kiasi kikubwa na safari ya Augustine Mrema mwaka 1995, baada ya kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa ndani ya chama wakati huo.

“Kuondoka kwa Lowassa ni sawa kabisa na Mrema, alipoamua kujiondoa CCM mwaka 1995. Aliondoka na watu walidai kuwa huo ndiyo ulikuwa mwisho wa chama lakini wapi? Kilishinda tena kwa kishindo na kimeendelea kushinda uchaguzi wote,” alisema Msekwa.

Aidha, Msekwa alisema kuwa umaarufu na nguvu walizokuwa nazo kina Lowassa na Mrema, zilitokana na uwepo wao ndani ya CCM na hivyo kuondoka kwao kumewafanya wasahaulike kwa haraka kwenye medani za siasa.

“Nguvu alizokuwa nazo Lowassa zilitokana na umaarufu mkubwa wa CCM. Si mnamkumbuka Samson wa kwenye Biblia? Yule bwana alikuwa na uwezo wa ajabu wa kupambana na kushinda watu zaidi ya 1,000. Hakukuwa na mtu aliyefahamu siri ya nguvu zake.

“Lakini baada ya maadui zake kumpeleleza kwa muda mrefu na kwa kutumia mwanamke aitwaye Delila, walifanikiwa kufahamu kuwa nguvu zake zilikuwa katika nywele hivyo wakamnyoa.
“Lowassa naye nguvu zake zilikuwa ndani ya CCM, hivyo muda si mrefu yatamkuta yaliyowakuta Mrema na Samson. Hatodumu katika umaarufu na nguvu alizokuwa nazo kama kipindi alipokuwa CCM,” alisema Msekwa.

Awali, Msekwa aliwataka Watanzania wawe na kumbukumbu ya enzi za Mrema alipoondoka CCM na watu wengi kumfuata kiasi cha baadhi yao kusukuma gari lake kwa ushabiki.

“Unajua watu hawataki kukumbuka matukio yaliyowahi kutokea, japokuwa si ya miaka mingi. Nakumbuka mwaka 1995, wakati Mrema akijitoa ndani ya CCM, maelfu ya watu walimshangilia na kumfuata alikokuwa akienda. Aliondoka na wanasiasa mashuhuri kama Wassira (Stephen), Marando (Mabere), Lamwai (Masumbuko) na Ndobho (Paul).”

“Lakini, cha kushangaza ni kwamba baada ya kuondoka nao na kudumu na umaarufu wake kwa muda usiozidi miaka miwili, yuko wapi leo? Si ajabu na hao mambo yaliyompata Mrema yakampata na Lowassa,” alisema Msekwa.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment