Videos

Sitta, Makinda kwenye mizania



* Kasi na viwango vya Sitta vilipitiliza, ikavuruga
* Makinda ajitolea kufunda wabunge vijana

Neema Mgonja
 
ALIYEKUWA Katibu Msaidizi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, John Joel amesema hakuna uhusiano wa karibu kati ya taaluma ya Sheria na Uspika wa Bunge, akitolea mfano wa uongozi wa Samuel Sitta ambaye ni mwanasheria na Anne Makinda.

Alisema kazi ya uspika inaongozwa zaidi na kanuni za Bunge na busara za Kiti cha Spika kuliko sheria, ndiyo maana Bunge la Sitta lilipitiliza na kufanya mambo yaliyoingilia kazi za Serikali ikilinganishwa na la Makinda.

Joel alitoa kauli hiyo alipozungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Dodoma hivio karibuni.

“Hakuna ulazima wa kuwa na Spika mwanasheria, uspika unaongozwa na kanuni, Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatoa nafasi kwa raia yeyote mwenye sifa za kugombea ubunge kugombea  uspika, na kanuni  zinatoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge.

“Busara ikitumika zaidi inakuwa ndiyo msingi wa kuongoza Bunge, wabunge ni watu ambao kila mmoja ana tabia zake, ukisema utumie sheria kwenye kila kitu, lipo tatizo la kuongoza wabunge kwa kuwa ni wanasiasa wanatakiwa kuwa huru. Ukiwabana sana wakati mwingine unaweza kupata Bunge ambalo si hai, ndiyo maana upo utaratibu wa kufuata kanuni.”

Hata hivyo, Joel ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema: “Faida kubwa ya kuwa na Spika mwanasheria – pengine ni wakati wa utungaji sheria. Labda hapo kwa wanasheria wanapata nafuu ya kuwa wanajua mambo mengi, lakini hata hivyo, bado Kiti cha Spika kina wataalamu wengi wakiwamo wa sheria ambao muda wote wanafanya kazi kumsaidia Spika.”

Utendaji wa Sitta

Akizungumzia utendaji wa Sitta aliyeongoza Bunge la tisa kwa miaka mitano, Joel alisema Sitta alijikita katika kuongoza Bunge kwa dhana aliyoijenga ya kasi na viwango.

Alisema kutokana na mtazamo huo, alijikuta Bunge aliloongoza likifanya kazi ambayo haikustahili kufanywa kwa kuwa lilikwenda mbele zaidi.

Joel alifafanua kuwa Sitta alikuwa na mtazamo wa Kasi na Viwango  na si mtazamo wa sheria, ila alitazama kufanya kazi kwa haraka na viwango.

“Bunge lake lilipitiliza, matokeo yake Serikali ikawa inabaki nyuma kulingana na mambo yaliyokuwa yakifanywa na Bunge, ikasababisha wabunge kufanya kazi isiyo yao, walianza kuingilia kazi za Serikali,” alisema.

Joel alieleza kuwa hayo yalisababishwa na Sitta kwa kuwa alitaka mambo yaende haraka na hata kusababisha Serikali kujikuta imeachwa nyuma.

“Unakuta wabunge wako kwenye vikao badala ya Serikali kuwa mtekelezaji, wabunge wanakwenda kuhimiza utekelezaji, walifanya kazi zisizo zao kabisa.

“Lakini hiyo ilitokana na mtazamo wa Sitta kutaka mambo ya kasi na viwango, kwa hiyo kwenye kuvutana huko kwenda na kasi lazima kuna aliyebaki nyuma, ndiyo yalifanya Serikali kuachwa nyuma,” alisema Joel.

Makinda  

Naibu Katibu huyo mstaafu akizungumzia utendaji kazi wa Spika wa Bunge la 10, Makinda alisema alijikita zaidi  kulea wabunge kwa maadili, huku akieleza kuwa alirudisha hadhi ya Bunge kwa kuliwezesha kujitegemea na kuachana na kasumba iliyokuwa imejengeka ya wabunge kupokea takrima na bahasha zisizo rasmi.

Kuhusu Spika huyo aliyehudumu katika Bunge kwa miaka 24 kabla ya kustaafu, alisema ingawa alikumbana na changamoto mbalimbali lakini alitumia muda mwingi kujenga Bunge, kwa kuelekeza wabunge kwenye maadili.

Huku akimwita ‘mama wa Bunge’, Joel alisema Bunge chini ya Makinda lilikuwa na changamoto nyingi hasa kwa kuwa ndicho kipindi ambacho kilikuwa na mabadiliko makubwa likishuhudia ujio wa wabunge wengi vijana.

Alisema ingawa vijana waliingia kwa kiasi kikubwa, alitumia ulezi kuwarudisha kwenye mstari unaotakiwa na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

“Katika uongozi wake, yeye alitaka kuwarudisha wabunge wajue wajibu wao kama wabunge, na mipaka yao ya namna ya kufanya kazi…Makinda alikuwa na mtazamo wa ulezi zaidi, tukumbuke kwamba tangu tulipoanza mfumo wa vyama vingi yalijitokeza mambo mengi.

“Zamani Bunge lilikuwa kwa watu waliostaafu na watu wasio na kazi, lakini baada ya mfumo wa vyama vingi na siasa kukua, ukaonekana umuhimu wa kuwapo kada mbalimbali, kwa hiyo Makinda akakutana na changamoto ya wabunge vijana,” alisema.

“Mtazamo wa Makinda hasa baada ya kuona yuko kwenye Bunge la vijana wakiwamo ambao hawakupata kufanya kazi kwingine na hiyo kuwa kazi yao ya kwanza, ilimfanya ajikute ameingia kwenye enzi za ulezi zaidi, akifundisha vijana maadili,”alisema Joel.

Takrima

Katika hatua nyingine,  Joel alisema Makinda tofauti na maspika waliomtangulia, alipenda Bunge liwe lijitegemee, ikiwa ni pamoja na kurudisha heshima na hadhi yake kama Bunge.

Alifafanua, kwamba kabla ya uongozi wa Makinda, Bunge lilikuwa na taratibu ya kuruhusu kupokea fedha kutoka nje, zikiwa ni gharama zilizokuwa zikilipwa kama takrima kwa wabunge, jambo ambalo Spika Makinda hakupendezwa nalo.

Aliongeza kuwa Makinda aliona utolewaji wa fedha za ziada kwa wabunge ambao pia walikuwa wakigharimiwa na mhimili huo, ni jambo ambalo halipendezi na linarudisha nyuma utendaji wake kiuadilifu.

“Awali wabunge walipokea bahasha sana, kwa mfano wakienda kutembelea sekta fulani walilipwa, siwezi kuita rushwa, lakini ni kama takrima hivi, jambo ambalo yeye akiwa Spika hakulikubali akaondoa huo mfumo wa kufadhiliwa,” alisema.

“Unajua mtu akikufadhili utataka kumfanyia mazuri, sasa unakuta wabunge wanakwenda kutembelea sehemu Fulani, wanapewa fedha na Bunge, na tena hiyo taasisi iwape fedha, ufanisi unakuwa si mzuri, kwa hivyo yeye Spika ambaye alikuwa na mtazamo tofauti alikuja na mbinu nyingine ya kukataa mifumo hiyo ya takrima kwa wabunge,” alisema Joel.

Mchango wa Sitta

Katika uongozi wake wa Bunge, Sitta aliyejulikana kwa jina la ‘Spika wa Kasi na Viwango’, Bunge lilibadili kanuni ambazo kwa mara ya kwanza kamati muhimu za fedha, ikiwamo ya Mashirika ya Umma, ya Fedha za Serikali Kuu na ya Serikali za Mitaa, zilisimamiwa na wenyeviti wa vyama vya Upinzani.

Baada ya kuundwa kwa kanuni hiyo, Bunge lilishuhudia vyama vya Upinzani kupitia kwa aliyekuwa Mbunge wa Karatu,  Dk Wilibrod Slaa (CHADEMA) na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), wakitumia kamati hizo kuimarisha upinzani ndani na nje ya Bunge kwa kuisulubu Serikali.

Mafanikio mengine yanayohusishwa na Sitta, ni pamoja na kuanzishwa kwa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, ambacho kilirithiwa na mabunge yaliyofuata baada ya uongozi wake.

Uongozi wa Spika huyo wa zamani, pia anatajwa kuwa ndio uliolipa Bunge uhuru mkubwa kiasi cha kufanikiwa kuiangushwa Serikali wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipolazimika kujiuzulu wadhifa wake sambamba na Baraza lote la Mawaziri.

Ni kutokana na uongozi huo wa Sitta, ndani ya CCM kuliibuka makundi yaliyohasimiana ambayo yalifikia hatua ya Sitta kunusurika kuvuliwa uanachama kwa kuonekana kuwa kiini cha msuguano wa makundi hayo, yaliyokuwa yakihatarisha umoja na mustakabali wa chama tawala.

Msuguano huo uliendelea hata Sitta alipotoswa kwenye kinyang’anyiro cha uspika hata wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete alipokiri kuwa kama CCM ilipita salama katika uchaguzi huo, basi itaendelea kudumu.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment